Mabomu yarindima bomoabomoa Dar






Operesheni ya uwekaji wa alama ya X kwenye nyumba zilizojengwa mabondeni, fukwe za bahari na maeneo ya wazi, jana ilikwama kwa saa tatu baada ya vijana kufunga njia kwa magurudumu yaliyokuwa yakiwaka moto kupinga hatua hiyo.


Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walijaribu kuwatawanya vijana hao kwa kufyatua mabomu ya machozi, lakini ilishindikana na ndipo walipotumia mazungumzo kuwaelewesha vijana hao ambao baadaye walikubali na kuruhusu kuendelea kwa operesheni hiyo ya kuweka alama nyumba zinazotakiwa zibomelewe.


Uwekaji huo wa alama unafanyika baada ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kutoa muda hadi Januari 5 kwa wote waliojenga kwenye maeneo hayo kubomoa nyumba zao kabla ya utekelezaji wa amri ya kuondoa makazi hayo kufanywa kwa nguvu, kwa mujibu wa mwanasheria wa baraza hilo, Manchare Suguta.


Jana, taharuki ilitanda kuanzia saa 4:00 asubuhi kwenye maeneo hayo na barabara inayotoka makao makuu ya klabu ya Yanga hadi kona ya Kigogo Darajani baada ya kufungwa kwa muda na vijana hao kabla ya askari hao kufika na kuanza kupiga mabomu ya machozi zaidi ya 15 kujaribu kuwatawanya.
Baada ya mabomu hayo, askari walikwenda kuzima magurudumu hayo, huku vijana wakionekana kutaka kukimbia.

Lakini ofisa aliyekuwa akiongoza askari hao aliwaita na kuzungumza nao kwa muda kabla ya kufikia makubaliano.

“Waacheni hawa wafanye kazi yao na hayo mengine yatashughulikiwa baadaye,” alisema kamishna msaidizi wa polisi, Ulrich Matei aliyeongoza askari hao na kuongeza kuwa: “Si vizuri tukaanza kuvunjana miguu bila ya sababu.”


Wakizungumza na Mwananchi baada ya sakata hilo kutulia, wakazi wa eneo hilo walisema wako tayari kuondoka, lakini wanataka kulipwa fidia ya nyumba zao.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilala Kota, Amin Iddy alisema kati ya wakazi 3,000 wa mtaa huo ni 45 tu waliopewa viwanja Mabwepande.

“Sasa inakuwaje wanataka kutuondoa bila kujua hatma yetu? Hatukubaliani na haki lazima itendeke, vinginevyo tuko tayari kwa lolote,” alisema.

Msimamizi wa operesheni hiyo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Charles Mkalawa, alisema hatua hiyo ni mwanzo wa utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwataka waliojenga na kuishi maeneo hatarishi, kuondoka ili kuepuka majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

“Hili ni eneo hatarishi na lilitangazwa hivyo tangu mwaka 1979 na wananchi wanaoishi hapa wanatakiwa kuhama,” alisema.

Takriban nyumba 8,000 zinatakiwa kubomolewa kwenye operesheni hiyo.

Wakati huohuo, Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema polisi imeanza msako wa kuwatafuta watu waliohusika na vurugu hizo za jana.

Alisema kutokana na vurugu hizo wameamua kuongeza askari katika operesheni hiyo ili kuwarahisishia kazi maofisa ardhi kutekeleza shughuli yao kwa ufanisi.


“Polisi inatoa onyo kwa watu watakaodiriki kuwasumbua maofisa ardhi katika zoezi la kuweka alama ya X. Atakayekiuka agizo hili tutakula naye sahani moja. Ni lazima sheria ifuate mkondo wake,” alisema Kova.
-Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment