LOWASSA:Mkiendelea na Mchezo wa Kupiga Watu Mabomu Tukimaliza Uchaguzi Tutawapeleka The Hague Mkakipate cha Mtoto na Huko Hamtarudi



Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.

Kutokana na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni takriban kilomita nane.

Katika hotuba yake iliyochukua dakika 14 kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema anawasikitikia wanaobeza nguvu hiyo ya umma.

“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.

Akizungumzia idadi hiyo ya wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema haijawahi kutokea maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

“Mwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,” alisema Regina.

Lowassa aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The Hegue.

“Nimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu asubuhi. Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The Hague mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,” alisema.

Polisi mkoani hapa jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa ambao walifurika Uwanja vya Ndege wa Mwanza kumpokea Lowassa.

Lowassa aliwasili akiwa ameambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.

Mabomu ya machozi yalianza kurindima saa tano asubuhi, baada ya baadhi ya wafuasi wa Ukawa kutaka kuingia kwenye lango la uwanja wa ndege, huku wengine wakijaribu kuwatunishia misuli polisi kwa kuwatupia mawe.

Hekaheka za mapokezi ya Lowassa zilianza saa mbili asubuhi, baada ya maelfu ya wafuasi wa Ukawa wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo: “Oil chafu ni kiboko ya mchwa” kutanda kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege.

Msafara wa Lowassa kutoka uwanja vya ndege uliongozwa na pikipiki ambazo zilikuwa zinapeperusha bendera za vyama vya CUF, Chadema ,NCCR Mageuzi na NLD, huku viongozi hao wakiwa kwenye magari ya wazi.

Lowassa alisema ziara yake hiyo inahusu kujitambulisha na asingependa kuwapa nafasi wapinzani wake kumtafsiri kuwa hajui sheria, lakini kero za Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi kurejea na mikakati ya kuzitatua.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment