Katika mitandao ya kijamii Jumamosi iliyopita kulisambaa picha za rapa Chidi Benz ambazo zinamuonyesha akiwa amedhorofika na kupoteza ule mwili wake wa kuvutia aliokuwa nao zamani.
Hivi ndivyo Chidi Benz alivyokonda sasa
Oktoba 24 mwaka 2014, Chidi alikamatwa na madawa ya kulevya katika Uwanja wa Ndege wa JK Nyerere wakati akielekea jijini Mbeya kwa ajili ya show. Lakini kesi hiyo ilimalizika miezi michache baadaye baada ya kuamriwa na mahakama kulipa faini.
Tukio hilo liliwafanya wasanii mbalimbali kuzungumzia hali hiyo huku wakimshauri kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya. Ray C ambaye ni mmoja kati ya waathirika janga hilo ambaye kwa sasa yupo kwenye tiba ya methadone, aliamua kumshauri Chid Benz.
“Pole kaka yangu Chidi Benz. Ninaumia kuona tatizo uliokuwa nalo bado haujalitafutia jibu la kutatua tatizo lako. Mimi ni dada yako na tumeshafanya kazi pamoja, tatizo ulilonalo na mimi nimewahi kua nalo na niliweza kulitatua sababu nilijitambua na kutafuta suluhu, nimejaribu kila njia kukushauri badala yake ukaja na rungu la kimasai na kunitandika nalo nyumbani,” aliandika Ray C kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Hata hivyo Chidi Benz aliendelea na harakati zake huku akijinadi katika vyombo vya bahari kwamba tayari ameshaachana na matumizi ya madawa ya kulevya. Lakini watu wake wa karibu, pamoja na marafiki zake walikuwa wanadai kwamba bado hajaacha. Jumamosi iliyopita, akiwa katika kipindi cha Da Weekend Chart Show ya Clouds TV, Chidi alionekana amechoka zaidi huku akiomba wadau mbalimbali wamsaidie.
“Matatizo yangu na stress zangu ambazo niko nazo zinanisababishia mwili wangu unapungua kwasababu siko okay, siko poa, siko sawa yaani,” alisema.
Mmoja kati ya wasanii wakongwe wa muziki wa Hip Hop, Afande Selle, alionyesha kusikitishwa na jinsi madawa ya kulevya yanavyomaliza nguvu kazi ya taifa. “Yanapita kwa njia gani madawa ya kulevya hapa nchini? Anayasambaza nani mitaaani kote mitaani? Madawa ya kulevya hayaleti maendeleoooo,madawa ya kulevya yanaua masela leooooo,” alisema Afande Selle.
Wadau mbalimbali wamewataka watu pamoja na wasanii wenzake kumsaidia huku Arnold Kayanda, mtangazaji wa BBC Swahili akisema amelipokea kwa masikitiko suala hilo.
“Kama picha hii ni rafiki yangu Chidi Benz kama nilivyotaarifiwa, kwa hisani yenu wote naomba kila mtu kwa nafasi yake amsaidie. Mimi niko mbali lakini nikirudi nitakutana naye,” alisema.
Licha ya wadau mbalimbali kutamka haja ya Chidi kupata msaada, bado tunaona hakuna juhudi za haraka ambazo mpaka sasa zimechukuliwa ili kumuokoa Chidi Benz.
Serikali ya Magufuli ni sikivu sana, na bila shaka kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inayoongozwa na Waziri kijana mpenda sanaa, Nape Moses Nnauye, tunatumai ataliangalia suala hili la wasanii kuangamia kwa madawa ya kulevya na kulipatia uvumbuzi.
0 comments:
Post a Comment