Magufuli ni zaidi…


Waandishi Wetu
HAIJAWAHI kutokea! Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kimezindua kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar huku umati wa watu waliojitokeza ukivunja rekodi kwa kukusanya wanachama na wananchi wengi kuliko katika kipindi cha rais Jakaya na Mkapa.
TATHMINI YA WATU WALIOHUDHURIA
Katika kile kilichotajwa kama zaidi ya mafuriko, ‘Tsunami’, umati uliohudhuria tukio hilo unakadiriwa kufikia maelfu kwa maelfu wakiwemo wananchi mbalimbali, wanachama wa CCM na wasanii mbalimbali wa muziki wa zamani na wa kizazi kipya, wamkiwemo waigizaji.
Wasanii waliokuwepo ni pamoja na Nasibu Abdul ‘Diamond’, Khadija Kopa akiwa na Kundi la Tanzania One Theatre, Yamoto Band, Steve Mengele ‘Steve Nyerere’, Single Mtambalike ‘Rich’, Wema Sepetu aliyeambatana na Yobnesh Yusuph ‘Batuli’, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, Khalid Ramadhani ‘Tunda Man’, Astelina Sanga ‘Linah’ na wengine kibao ambao baadhi yao walionesha uwepo wao kwa kutumbuiza nyimbo mbalimbali jukwaani.
MAMBO YAANZA
Ishu nzima ilianza saa 7 mchana ambapo wasanii mbalimbali walipanda jukwaani kutoa burudani likiwemo kundi la TOT, Vijana Jazz, Bendi ya Walemavu na wakafuatiwa na Yamoto Band kisha msanii wa Mnanda, Easy Man, Bushoke na akaingia Peter Msechu. Baadaye ilikuwa ni zamu ya Rais wa Wasafi, Diamond ambaye alifunga duru kwa upande wa burudani huku shoo yake ikinogeshwa na gwiji wa komedi nchini, Amri Athman ‘Mzee Majuto’.
WALIOTIA FORA
Baadhi ya wasanii walitia fora kwa kubadili nyimbo zao na kuwa zenye kukisifia chama hicho ambapo, Diamond aliubadilisha wimbo wake wa Number One, Yamoto Band nao waliubadilisha wimbo wao wa Niseme Nisiseme. Halikadhalika Peter Msechu ambaye aliubadili wimbo wake wa Nyota.
SALAMU ZA WAWAKILISHI
Baada ya burudani, Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye aliwakaribisha baadhi ya wawakilishi kutoka vyama vya siasa, na makundi mbalimbali ya kijamii ambapo wafanyabiashara ndogondogo ‘Wamachinga’ nao walitoa salamu zao kupitia kwa mwenyekiti wao huku waendesha pikipiki ‘bodaboda’ nao wakiwakilishwa na mwenyekiti wao.
MAKONGORO NYERERE AWA KIVUTIO
Mmoja wa watangaza nia ambaye naye alikatwa katika kinyang’anyiro cha urais wa chama hicho, Makongoro Nyerere ambaye alipewa nafasi ya kuwakilisha familia ya muasisi wa taifa la Tanzania, Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, alionekana kuwa kivutio kutokana na vijembe mbalimbali alivyowapiga Ukawa.
“Tutawapiga tobo si wametaka wenyewe, maana kama mzee kaingia mchezo wa vijana mnategemea mimi nifanyaje! Nitampiga tobo na akigeuka nitampiga kanzu. Miwani Oyeeee, Kofia Oyeeee, Kifimbo oyeee,” alisema Makongoro na kuamsha shangwe ya kutosha kutoka kwa wana- CCM.
WALIOZUNGUMZA
Baadhi ya viongozi waliofanikiwa kutoa salamu zao ni, Waziri Mkuu Mstaafu (Jaji Joseph Warioba), Rais Mstaafu Awamu ya Pili (Ali Hassan Mwinyi), Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu (Benjamin Mkapa), Katibu Mkuu wa CCM (Abdulrahman Kinana) na kumaliziwa na Rais Jakaya Kikwete.
MKAPA AWAPA MAKAVU LAIVU
Katika hatua nyingine, rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwapa ‘makavu laivu’ Ukawa akisema ni watu wasiokuwa na hoja katika siasa ya vyama vingi na wamejaa uchu wa madaraka huku Jaji Warioba yeye akimmwagia sifa kibao mgombea wa chama hicho, John Magufuli ‘JM’.
MAGUFULI AFANYA YAKE
Naye John Magufuli ambaye ndiye mlengwa wa uzinduzi huo, alifungua kampeni zake kwa kutoa ahadi kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji huku akilenga kufanya mabadiliko kwa walimu, mama lishe, wafanyabiashara ndogondogo, wanafunzi, hasa suala la mikopo na suala la ajira sambamba na kumtambulisha mke wake, Janet Magufuli.
Katika uzinduzi huo aliyekuwa mgombea wa Chadema katika Jimbo la Sikonge, Said Nkumba alirejea CCM ikiwa ni siku chache alipotangaza kujiunga na chama hicho cha upinzani.
Stori: Richard Bukos, Gabriel Ngo’sha, Chande Abdallah, Deogratius Mongela na Shani Ramadhani.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment