Picha: Kilimanjaro Premium Lager yakabidhi vifaa kwa Simba na Yanga


Bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayodhamini vilabu vikongwe vya Simba na Ynaga imekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya milioni 70 kwa vilabu hivyo vitakavyotumika katika msimu wa Ligi Kuu unaotarajiwa kuanza Septemba 12 mwaka huu.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa na meneja wa Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli jijini Dar Es Salaam leo.

Vifaa hivyo ni pamoja na jezi za mechi seti mbili kwa kila klabu, jezi za mazoezi, casual wear, mipira, sheen guard, viatu vya kuchezea mechi, viatu vya mazoezi, soksi, gloves za makipa na mavazi ya mabenchi ya ufundi.

Akikabidhi, Pamela amesema ni matumaini yake kuwa vilabu vyote viwili vitatunza vifaa vizuri na wachezaji watatumia vifaa vinavyohitajika katika sehemu husika. “Mchezaji hategemewi kwa mfano kusafiri na malapa au mavazi tofauti na yale yaliyotengwa kwa kusafiria na yenye nembo ya mdhamini”, alisema.

Alisema pamoja na kutoa vifaa kila mwanzo wa msimu, Kilimanjaro Premium Lager imeendelea kuhakikisha mishahara ya wachezaji inalipwa kwa wakati na pia ilinunulia vilabu vyote viwili mabasi ya kisasa ambayo vilabu vitatumia kusafiri na kwa masuala mengine yanayohusu wachezaji.

Katika hatua nyingine alitoa pongezi kwa Simba na Yanga kwa kumaliza katika nafasi nzuri katika ligi kuu ya Voda msimu uliopita. Yanga waliibuka na ushindi huku Simba wakiwa wa tatu.

“Sisi wadhamini tunapenda kuona ushindani ukiwa mkubwa mno na timu zote mbili zilenge kunyakua taji la ligi kuu na mataji mengine katika mashindano ya kimataifa.

Alitoa changamoto kwa Simba ijitahidi msimu ujao iweze kushika nafasi ya kwanza au ya pili ili icheze mashindano ya kimataifa kama wenzao Yanga. Simba haijashiriki mashindano haya kwa misimu takribani minne sasa.

“Timu zote zimesajili vizuri na hii imejidhihirisha wazi kwani Simba hawajashindwa mechi hata moja tangu kufika kwa kocha mpya na Yanga pia wameshinda ngao ya hisani. Hii inadhihirisha kuwa msimu ujao utakua na ushindani mkubwa kwa hivyo timu zote mbili zianze kwa matokeo mazuri”, alisema Pamela.

Alisema vilabu hivi vinapofanya vizuri ni fahari kwa wadhamini kwani wanapata faida ya udhamini na kusisitiza kuwa Kilimanjaro Premium Lager ina lengo la kufikisha mpira wa Tanzania katika kilele cha mafanikio na ndio maana pia imejikita katika udhamini wa timu ya taifa, Taifa Stars.







Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment