Kortini kwa mauaji ya polisi na raia Stakishari
Idadi ya washtakiwa waliofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka saba ya mauaji ya maofisa wanne wa polisi na raia watatu katika kituo cha jeshi hilo cha Stakishari, imeongezeka hadi kufikia 10.
Wakili wa Serikali, Hellen Moshi jana aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Omari Makota (28); Rajabu Ulatule (22); Ramadhani Ulatule (20); Fadhil Lukwembe (23) na Ally Salum (63).
Wengine ni Hamis Salum (51); Nassoro Abdallah (42); Seleman Salum (83); Said Mohammed (67) na Said Abdullah Chambeta ‘Mzee wa Fasta’ (45).
Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mauaji hayo Julai 12, 2015 kinyume na Kifungu cha 196 ya Sheria ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Moshi aliwataja polisi waliouawa kuwa ni Sajenti Adam, Koplo Gaudini, Koplo Peter na Konstebo Anthony. Raia ni Salehe Simkoko, Erick Wangandumi Swai na Jackline William Duma.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote hadi watakapofikishwa Mahakama Kuu baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
0 comments:
Post a Comment