Rais John Magufuli jana alituma ujumbe mzito katika mapambano dhidi ya rushwa nchini, akisema mapambano hayo ndiyo mwelekeo wake na hatabadilika hata kama itakuwa ni kutoa sadaka mwili wake.
Alitoa ujumbe huyo alipofungua mkutano wa wakandarasi jijini Dar es Salaam, akiendelea na ‘kampeni yake’ ya kuhimiza uzalendo na kupambana na ufisadi.
“Na bahati nzuri nashukuru, Watanzania wananiombea na Mungu ananisimia kwa sababu nafahamu kazi hii zikupewa na mtu, nilipewa na Mungu,” alisema Rais huku akipigiwa makofi.
“Na watu wanaoteseka ni watu wa Mungu, hasa watu maskini. Ni lazima nitimize wajibu wangu, hata kama ni kwa kutoa sadaka yangu, sadaka ya mwili wangu.”
Magufuli hakuwa anapewa nafasi ya kupitishwa na CCM kuwania urais, lakini upepo ulibadilika ghafla baada ya jina la Edward Lowassa kukatwa na kubakia makada watano. Magufuli aliongoza kwenye kura za Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu na kushinda urais katika kinyang’anyiro kilichokuwa na ushindani mkali
Tangu aingie madarakani amekuwa akieleza jinsi nchi ilivyofikishwa pabaya kutokana na wizi, ufisadi, uzembe na matumizi mabaya ya fedha za umma na amepambana na wafanyabiashara wakubwa katika masuala ya ulipaji kodi.
Akiwa mapumzikoni jimboni kwake Chato, Rais alinukuliwa akisema angejua urais ulivyo asingejitokeza, lakini akaahidi kuendelea na mapambano.
Jana Magufuli ambaye aliambatana na mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, aliendelea kusisitiza msimamo wake wakati akizungumzia suala la makandarasi wazalendo kuweka viwango vya juu vya fedha wakati wanapoomba zabuni serikalini.
Na ndio maana nawaomba sana wakandarasi, sana. Tubadilike kwa ajili ya nchi yetu,” alisema.
“Unapoona watu wanashangaashangaa sana (ni) kwa sababu hawakuzoea haya. Na walifikiri nitakuwa part of them (sehemu yao), never (haitatokea), not me (si mimi)
“Ni mara 10 nisiwe rais, nikachunge hata ndege, nikakae kijijini kuliko niwe Rais halafu nivumilie uozo huu unaofanyika. I’m saying never (nasema haitatokea).”
Rais alisema ataendelea na vita aliyoianzisha na atawashughulikia kikamilifu wanaofanya uovu huo.
“Kama ni kutumbua kila siku nitatumbua tu. Watu lazima wabadilike. That is my direction and I will never change it (huu ndiyo mwelekeo wangu na sitaubadili).”
Akieleza sababu ya kuambatana na Mlowola, Rais Magufuli alisema anataka ashirikiane naye katika kupambana na rushwa katika sekta hiyo ya wakandarasi.
“Mlowola nina uhakika hawajakualika, lakini nimekuchukua ili kusudi tushiriki mimi na wewe kwenye kikao na sifahamu kwa nini mwenyekiti hakukualika,” alisema Rais Magufuli.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment