Teknolojia ya kutumia viungo vya maiti yanukia Tanzania


Mapinduzi ya tiba yanaashiria kuwa viungo vingi vya mtu aliyekufa vinaweza kuhitajika kwa ajili ya kuwakarabati watu ambao wamepata ajali na kupoteza viungo au wanaolazimika kukatwa kwa sababu ya maradhi.


Hii ni teknolojia ya kisasa ya kitabibu ambayo ni ya kutumia viungo vya maiti kuoka maisha ya wengine.

Gari ikiharibika kiasi ambacho haitengenezeki, huwa halitupwi. Kinachofanyika ni kuondoa baadhi ya vifaa muhimu ili vitumike kama vipuri kwa magari mengine yakiharibika.

Kukomaa kwa taaluma ya matibabu kunafanya mifumo ya tiba ibadilike na kuwa sawa na huo wa matumizi ya magari.

Mapinduzi ya tiba yanaashiria kuwa viungo vingi vya mtu aliyekufa vinaweza kuhitajika kwa ajili ya kuwakarabati watu ambao wamepata ajali na kupoteza viungo au wanaolazimika kukatwa kwa sababu ya maradhi.

Hospitali za Apollo nchini India zimeanza kujijengea umaarufu kitabibu katika kutumia teknolojia ili kuboresha maisha ya watu.

Matukio yaliyofanyika Mei 4, mwaka huu, chini ya Hospitali Kuu ya Apollo Chennai, India, ilishuhudia timu ya madaktari ‘ikivuna’ viungo 23 tofauti vya mwili.

Viungo hivyo ni figo 10, macho pea tatu, mioyo miwili na maini mitano.

Utofauti wa tukio hili pengine ni kuwa ni mara ya kwanza familia tano zilizofiwa, kujitokeza na kukubali kujitolea viungo vya mwili wa mpendwa wao marehemu ili kuokoa maisha ya wengine.

Viungo hivi kwa kawaida huondolewa punde mgonjwa anapobainika amefariki. Tendo hili limeushangaza ulimwengu wa kitabibu na katika mchakato huu kuweka rekodi ya kiasi kikubwa cha viungo kuwahi kuvunwa kwa siku moja.

Timu ya madaktari 100 wenye taaluma mbalimbali ilitumia sehemu saba za vyumba vya upasuaji kwa wakati mmoja kuvuna viungo 23 na kufanya upandikizaji wa viungo 10 kwa wakati huohuo.

Madaktari na wafanyakazi wasaidizi walifanya kazi kwa saa 12 kusaidia tukio hili la kukumbukwa, iliyoongeza tena sifa nyingine kwa mafanikio ya Hospitali za Apollo katika kuendesha shughuli nyingi zaidi za upandikizaji viungo duniani.

Katika kupongeza ukarimu wa familia zilizojitolea, Hospitali za Apollo ziliandaa sherehe kwa lengo la kuelezea shukrani zao kwa familia hizi. Sherehe ilihudhuriwa na mwanzilishi na mwenyekiti wa Hospitali za Apollo, Dk Reddy, Makamu Mwenyekiti, Preetha Reddy na timu yote ya madaktari ambao walihusika katika kuhakikisha mafanikio ya mchakato huu.

Dk Reddy anasema: “Leo, familia hizi zenye nia njema zimesaidia kuwapa nafasi nyingine ya kuishi watu walio katika hatua za mwisho kwa viungo vyao kushindwa kufanya kazi. Ni kitendo kitakacho wahamasisha watu wengi zaidi kuchangia viungo.

“Inahitaji dhamira ya ziada kiubinadamu na kupevuka kwa dhamira ya uwajibikaji wa familia kuzisaidia jamii, hospitali na madaktari kutoa nafasi mpya ya maisha kwa wale wanaohitaji.

“Uhai wa binadamu haununuliki na maisha ya mtu yanapoweza kutoa uhai na matumaini kwa wengine wengi wanaohitaji; kwa hakika hakuna cha kulipia.”

Viungo vya maiti Tanzania

Watanzania wengi katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakitafuta huduma za kitabibu zaidi nchini India sababu ya maendeleo na urahisi wa huduma hizi nchini humo.

Kwa sasa Tanzania mpango wa kujitolea viungo halipo, labda hadi iundwe sera na taratibu za mchakato huu katika nchi kutasaidia watu wengi. Nchi kama India wanafaidika kwa kuwapo kwa sera hii inayoruhusu watu kufaidika kwa ukarimu wa wanafamilia wa marehemu kujitolea viungo vya mpendwa wao au marehemu mwenyewe kujitolea.

Uwezekano wa uvunaji viungo vya maiti hapa nchini unawezekana ukatumika miaka michache ijayo kutokana na mpango wa Hospitali za Apollo kuwa na mkakakati wa kujenga hospitali ya kisasa nchini.

Hospitali hiyo itakuwa na huduma sawa na zinazotolewa nchini India kwa lengo la kupunguza wimbi la wagonjwa kusafirishwa kutibiwa katika bara hilo la Asia.

Rais Jakaya Kikwete alipotembelea India Juni mwaka huu alisisitiza uendelezaji wa utekelezaji wa makubaliano yaliyopo ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Hospitali za Apollo.

Hospitali hiyo ya kisasa, ujenzi wake unatarajia kuanza wakati wowote eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam pamoja na kliniki ya uchunguzi inayotarajiwa kuwa katika jengo la NSSF, makutano ya Barabara ya Morogoro na Bibi Titi.

Hospitali za Apollo zimekuwa zikitia fora duniani katika kufanikisha upandikizaji wa viungo. Ni kitovu kikuu cha rufaa na mara nyingi Watanzania wamekuwa wakienda huko baada ya matibabu hayo kuonekana kushindikana nchini.

Hospitali za Apollo hivi karibuni zilipata tuzo ya dhahabu ‘Golden Peacock’ kutoka taasisi ya wakurugenzi, kwa kushirikiana na kitengo cha sera na uendeshaji, Serikali ya India. Hii ni tuzo ya juu zaidi ya ubora wa biashara katika sekta ya afya na kuchukuliwa kama kipimo cha kiwango katika tuzo za ubora wa kampuni.
-Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment