Tundu Lissu Ajibu Mapigo.......Asema Mwenye Richmond ni Rais Kikwete Mwenyewe


Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amtaje mhusika wa Richmond anayezunguka naye kwenye kampeni, Mbunge huyo wa Singida Mashariki ameibuka na kudai kuwa Rais huyo ndiye mhusika kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuteua na kuwawajibisha mawaziri.

Juzi, akiwa Kigoma, Rais Kikwete alieleza kumshangaa Lissu kumtaka amtaje mhusika wa Richmond wakati mtu huyo anazunguka naye kwenye mikutano ya kampeni na kumtaka amtaje la sivyo yeye (Rais), atamtaja.

Akihutubia mkutano wa kumnadi mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, mwanasheria hiyo alianza kwa kusema: “Sasa ndugu zangu naomba leo nimjibu Kikwete na tumalizane na hii habari ya Richmond."

Alisema mkuu huyo wa nchi ndiye mhusika kutokana na mamlaka yake na; “si ya huyu Lowassa anayedai natembea naye kwenye kampeni. Hapa kwenye mkono wangu nina taarifa ya mwaka 2008 ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe, sasa ni miaka zaidi ya saba tangu isomwe bungeni.”

Lissu aliyekuwa akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo katika viwanja vya shule ya kiwanja cha ndege, alinukuu maelezo ya taarifa ya Mwakyembe kifungu kwa kifungu na kueleza namna ambavyo taarifa hiyo haikuweza kumtia hatiani Lowasa, bali aliwajibika kutokana na makosa ya watendaji wake.

Baada ya kueleza kwa kina taarifa hiyo, Mwanasheria huyo alisema Rais Kikwete ndiye pekee mwenye mamlaka ya kuwateua mawaziri, akisema alimteua Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha na ndiye mwenye mamlaka ya kuwawajibisha.
 
 Karamagi na Dk Msabaha walikuwa wameshika uwaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti wakati wa sakata la Richmond na walijiuzulu pamoja na Lowassa.

“Waziri mkuu Lowassa baada ya kutokea kwa sakata hilo alimwendea Rais Kikwete na kumweleza kuwa ‘kimenuka’ tuvunje mkataba baada ya wabunge wa upinzani kuchachamaa kuhusu sakata hilo, lakini alikataa na kumweleza kuwa hizo kelele za wapinzani zitaisha tu,” alisema.

Alisema baada ya Lowassa kujiuzulu mwaka 2008, tayari mashine za kutengeneza umeme zilishafika nchini na baada ya kujiuzulu haikufahamika zilikokwenda na kwamba baadaye mkataba wa Richmond ukahamishiwa kwa kampuni ya Dowans ambayo iliendelea kulipwa mabilioni ya shilingi.

Alimtaka Rais Kiwete awaambie Watanzania kwa nini Serikali yake iliendelea kuilipa Dowans mabilioni ambayo ilikuwa ya mfukoni na kwamba kama Lowassa alifanya makosa kwa nini hajapelekwa mahakamani kwa miaka minane tangu ajiuzulu.

“Rais Kikwete asitake kumaliza hizi siku chache za kampeni zilizobaki kwa shari na mimi na naomba niwaambie, Lowassa amefanya kazi katika umri wake wote wa miaka 62 ndani ya CCM na Serikali yake, lakini ameamua kuhamia huku kwa ajili ya kuleta mabadiliko na kuacha marupurupu yake yote,” alisema Lissu.

Msikilize Tundu Lissu Akiongea Hapo Chini.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment