Kituo cha treni chafunguliwa Budapest




Wahamiaji wakiabiri treni mjini Budapest
Kituo kikuu cha reli katika mji mkuu wa Hungary, Budapest, kimefunguliwa na mamia ya wahamiaji wameruhusiwa kuingia baada ya kufungwa kwa siku mbili.

Watu wengi wameonekana wakiingia kuelekea maeneo ya kusubiri treni katika kituo hicho baada ya milango kufunguliwa.

Lakini tangazo limetolewa kwa umma likisema safari za treni za kimataifa kuelekea Ulaya Mgagharibi zimesimamishwa "kwa muda usiojulikana".

Hayo yamejiri huku Waziri Mkuu wa Hungary, anayepinga wahamiaji Viktor Orban, akitarajiwa kutua Brussels kwa mashauriano ya kutafuta suluhu ya mzozo huo.

Wahamiaji waliokuwa wamekwama katika kituo cha treni cha Keleti, mjini Budapest, walizuiwa kuabiri treni siku ya Jumanne na Jumatano.
Baadhi walikabiliana na polisi.

Walikuwa wamenunua tiketi baada ya Hungary kuonekana kuachana na juhudi za kuwasajili wahamiaji hao kwa muda na kuruhusu wengi wao kuabiri treni na kuelekea Vienna, kusini mwa Ujerumani.

Haijaeleweka mara moja ni kwa nini watawala wameamua kuwaruhusu wahamiaji waingie kituo hicho cha reli leo asubuhi.

Wengi wamejaribu kujisukuma ndani ya treni iliyokuwa imeorodheshwa kwamba ingeondoka kuelekea Munich, lakini mwandishi wa habari wa BBC, Nick Thorpe, akiripoti kutoka kituo hicho anasema habari zimeanza kuenea kwamba hawataruhusiwa kusafiri kwenda Ujerumani.

Ujumbe kwenye bango la matangazo umesema tiketi za safari za kimataifa zitakubalika katika treni zinazohudumu ndani ya taifa hilo.

Idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya imeongezeka pakubwa na kuvunja rekodi, Julai pekee mwaka huu wahamiaji 107,500 waliwasili.

Ujerumani inatarajia kuwapokea wahamiaji 800,000 mwaka huu mara nne ya jumla ya wahamiaji iliopokea mwaka jana.

Ongezeko la idadi hiyo limesababisha kuwepo kwa mtafaruku na kutoelewana kuhusu sera ya uhamiaji Muungano wa Ulaya, EU.
Viongozi wa Ulaya watofautiana

Siku ya Jumatano, Ujerumani, Italia na Ufaransa ziliitisha kuwepo kwa "usambazaji wa usawa" wa wahamiaji kote Ulaya.

Italia na Ugiriki zimelalamika kwamba zinalemewa na idadi kubwa ya wahamiaji wanaowasili katika fuo zao.

Na ingawa nchi kama vile Ujerumani ziko tayari kupokea idadi kubwa ya wahamiaji, mataifa mengi hayako tayari.Wahamiaji wakivuka mpaka na kuingia Hungary
Mawaziri wa masuala ya ndani na haki wa nchi wanachama wa EU, watakutana Brussels Septemba 14 kujadili suala hilo.

Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alisema kupokea wakimbizi "zaidi na zaidi" si suluhisho.

Maafa ya kibinadamu yanayotokana na mzozo huo yalidhihirika wazi siku ya Jumatano pale ilipobainika kuwa watoto watano walikuwa miongoni mwa wahamiaji 12 waliokufa baharini Uturuki wakijaribu kufika Ugiriki.

Picha za mwili wa mvulana wa miaka mitatu uliopigwa na mawimbi ya bahari na kufikishwa ufuoni, baada ya kufariki pamoja na mamake na kakake wa miaka mitano, zilisambaa sana mitandao ya kijamii.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment