Natasha akerwa na utovu wa nidhamu kwa waigizaji wa kike


Mwigizaji huyo mkongwe amebainisha kwamba hayo ni matokeo ya walio wengi kuingia kwenye fani pasipo kupitia mafunzo.

Mwigizaji mkongwe wa filamu nchini Natasha Mamvi amesema utovu wa nidhamu na maisha yaliyojaa ukakasi kwa waigizaji wa kike hivi sasa, ni matokeo ya kuingia katika fani pasipo kupitia mafunzo ya taaluma hiyo.


Natasha, ambaye ni mzazi wa Monalisa, amesema kati ya vitu ambavyo humuumiza kichwa katika tasnia ya filamu ni namna maisha ya wasanii wa kike yalivyo na jinsi wanavyojishusha.

“Kile kitu ambacho unakiona ni kinyume na filamu, ujue huyo mtu hajapita katika mafunzo,” alisema. “Zamani kila tulipoingia kwenye makundi, kitu cha kwanza kabisa ilikuwa tunafundishwa nidhamu kama msanii na kama mtoto wa kike.

“Tulikuwa na watu wazima ambao walikuwa wanatuangalia na kutushauri au kukataza tabia fulani. Ilikuwa ukifanya kitu unaambiwa aah hicho kiache wewe ni msanii kioo cha jamii.”

Anasema kwa kuwa wengi hawajapata mafunzo hayo, yanayotokea sasa ni majibu ya kile ambacho kiliharakishwa kwa kisingizio cha kuwa na kipaji. “Kwa sababu wengi hawajapita katika mafunzo kama hayo, ndiyo maana leo hii haya yote yanatokea. Kuvaa nguo zisizo na staha, kuzungumza maneno yasiyo na staha, kukaa kwenye maklabu mpaka saa mbaya na hata kutengeneza skendo, ni vitu ambavyo unaona kabisa kwamba huyu mtu amekosa mafunzo,” alisema.

Natasha alisema awali wasanii walikuwa wakipitia kwenye vikundi na kujifunza misingi ya sanaa, tofauti na ilivyo sasa.

“Kwa mfano hivi sasa ukimchukua mtu ukaenda naye location (eneo la kuchukulia picha za filamu) unaweza kushangaa huyu ni msanii maarufu lakini mbona ABC hazijui? Na ukimwambia kwamba anakosea anakuwa mkali. Basi unamwangalia tu,” alisema.

“Nakumbuka kuna kipindi chipukizi waliniita kwa ajili ya kutengeneza filamu. Nikamuona mpigapicha anakosea kuchukua picha, nilipojaribu kumwambia akanuna. Nikashangaa kwa kuwa mimi nimekaa muda mrefu kwenye sanaa nilihitaji kumfahamisha lakini hakunielewa. Hapa ndiyo unaona aah kumbe kutokuingia kwenye vikundi au kupata yale mafunzo ya mwanzo kunasumbua tasnia yetu.”

Natasha, ambaye jina lake halisi ni Suzan Lewis, anafafanua kwamba ndiyo maana leo hii waigizaji wa kike wanajiachia hadharani bila kujali nini wanafanya na hata kutumia vibaya ya mitandao ya kijamii.

Anasema bado hajafanikiwa kuwapa elimu ya namna ya kujichunga.

“Hicho ni kitu ambacho sijawahi kukaa na kuzungumza nao. Siyo kitu cha kistaarabu. Wewe kama mwigizaji wa kike lazima ujue kwamba una wafuasi wangapi katika ukurasa wako wa mtandao wa kijamii. Lazima ujijue kwamba wewe ni maarufu na ujue kwamba unachokiandika kinamfikia nani na kitawavutia vipi watu au kuwakera.

“Mtu unaweza ukaandika mambo poa, mtu anaanza kujiuliza mambo poa ile ishu ya jana. Yaani neno dogo lakini kila mtu atatafsiri kitu chake, lakini unaweza kukuta mtu anakurupuka na kuandika kitu mtandaoni mpaka ukashtuka. Jaribu kuangalia mara mbili kile kitu unachoandika kina manufaa gani, siyo kitu cha kufundishwa ila ni umakini wa mtu mwenyewe,” alisema Natasha.

Natasha pia alizungumzia sababu za wasanii Bongo Movie kuchelewa kwenda Zanzibar kwenye tamasha la Ziff.

“Hiyo inatokana na vitu viwili kwanza ni gharama ya mtu, gharama zake zinamtosha kukaa siku zote Zanzibar, lakini kingine ni ratiba za mtu mwenyewe. Je ana nafasi ya kukaa Zanzibar kwa siku zote?

“Kitu kingine ambacho nimezungumza na kaimu mkurugenzi wa Ziff (Daniel Nyalusi), tujitahidi safari ijayo tufanye kama ni sikukuu ya wasanii, yaani ikianza ile siku ya kwanza yaani Swahiliwood yote ihamie Zanzibar hata kama huku Ziff watatulipa siku tatu za mwisho, sisi tutajenga kitu fulani,” alisema Natasha.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment